Maafisa wawili toka Umoja wa Afrika, Dkt Monica EbeleIdinoba na Bi Khadidiatou, walitembelea Kituo cha Kudhibiti Viumbe Hai Waharibifu, SUA, kwa siku mbili, tarehe 25 hadi 26 mwezi Machi, mwaka 2019. Lengo lilikuwa kujionea maendeleo ya mradi wa udhibiti wa panya unaofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya kupitia Umoja wa Afrika (AU).
Mradi huu wa miaka minne (2018 – 2022) unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya SUA na taasisi nyingine ndani na nje ya bara la Afrika. Mradi huu unalenga kuboresha na kuhamasisha matumizi ya njia mbadala za kupunguza athari zitokanazo na panya. Mifano ya njia hizo ni pamoja na matumizi ya vizuia uzazi (fertility control hormones), bundi na mifuko maalumu ya kuhifadhia nafaka ‘hermetic bags’. Tafiti za mwanzo zilizofanywa na timu ya watafiti katika Kituo cha Kudhibiti Viumbe Hai Waharibifu ikiongozwa na Prof. Rhodes Makundi, zimedhihirisha uwezo mkubwa wa kudhibiti idadi ya panya na athari zake kwa kutumia homoni zenye uwezo wa kupunguza kuzaliana kwa wanyama hao. Aidha, kwa kupitia kituo hiki, tafiti zimedhihirisha uwezekano wa kudhibiti panya kwa kutumia Bundi ambao wanategemea wanyama hao kama chanzo kikubwa cha chakula chao. Matumizi haya, yanahusisha kutengeneza viota pembezoni mwa mashamba vinavyovutia kuishi na kuzaliana kwa bundi.
Kwa kupitia mradi unaoendelea kwa sasa, teknolojia tajwa na nyinginezo zitaendelea kufanyiwa majaribio ndani ya Tanzania nchi nyinginezo ndani ya Afrika kama Namibia, Uganda, Afrika kusini, Eswatini na Ethiopia.
Wafanyakazi wa SPMC wakiwa katika picha ya Pamoja na wageni wa Umoja wa Afrika