Watafiti kutoka Taasisi ya Udhibiti wa Viumbe Hai Waharibifu SUA wametoa mafunzo ya udhibiti wa mazalia ya mbu na matumizi sahihi ya vyandarua vyenye dawa katika Kijiji cha Unone wilayani Kilosa, Mkoani Morogoro.
Mafunzo haya yaliyobeba kauli mbiu inayosema “Tumia Chandarua Bora Chenye Dawa Kuzuia Ugonjwa wa Malaria”. Hii ikiwa ni muendelezo wa tafiti zilizoanza kufanyika katika wilaya ya Kilosa hususani kwenye vijiji venye visa vingi vya ugonjwa wa malaria.
Watafiti wakishirikiana na viongozi wa Kijiji cha Unone ambao ni Mtendaji, Mwenyekiti wa kijiji na wenyeviti wa vitongoji walihamasisha jamii kuongeza juhudi za kutumia vyandarua kwenye kila kaya na pia kuzuia kuzaliana ya mbu kwenye makazi. Pia, watafiti wakishirikiana na waalimu wa shule ya msingi Unone kutoa mafunzo juu ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Malaria kwa wanafunzi.
Zoezi lilianza kwa kuwapima uelewa wanafunzi kuhusu ugonjwa wa malaria kwa kujaza dodoso. Dodoso hii ilikuwa na maswali mbalimbali ya uelewa kuhusu malaria, njia za kujikinga na malaria,matumizi ya chandarua chenye dawa n.k.
Wanafunzi walioshiriki katika kujaza dodoso ni wanafanzi wa darasa la nne, tano, na la sita ikiwa ni jumla ya wanafunzi 267, wasichana 154 na wavulana 123. Zoezi hili lilifanywa na watafiti kutoka Taasisi ya Udhibiti wa Viumbe Hai Waharibifu kwa kushirikiana na Mwl.Mkuu wa shule ya msingi Unone Mwl. Sostenes Msebi Dimoso.
Baada ya kujaza dodoso wanafunzi wote walikusanyika kupata elimu juu ya Ugonjwa wa Malaria, namna sahihi ya kufua chandarua , ushonaji wa chandarua chenye matobo na njia ya kudhibiti mazalia ya mbu maeneo ya Jirani na makazi ya watu.
Akiongea wakati wa utoaji wa elimu Mtafiti Dr. Amina Issae alisema Lengo la kutoa elemu ya ugonjwa wa malaria katika shule ya msingi ni kwamba wanafunzi wa shule za msingi ni mawakala wazuri wa kusambaza taarifa kwenye jamii. Hivyo, elimu ya kujikinga dhidi ya magonjwa ikitolewa kwa watoto wa shule inaongeza uelewa katika kizazi kipya na pia, kufikisha taarifa kwenye jamii hususani wazazi, walezi, ndugu , jamaa na marafiki kwa ujumla.