Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Nchini Tanzania Bw. Nathan Belete amepongeza Kituo cha Umahiri cha Mashariki na Kusini mwa Afrika cha kudhibiti panya na matumzi yake katika kunusa (ACE IRPM & BTD) kwa kutumia fedha zilizotolewa na Benki hiyo kama ilivyokusudiwa.
Mkuu wa Kituo cha Umahiri cha Mashariki na Kusini mwa Afrika cha Utafiti na Udhibiti panya na matumzi yake katika kunusa Prof Apia Massawe aliweza kutoa wasilisho la shughuli mbalimbali zilizotekelezwa nazinazoendelea kutekelezwa na kituo hiki pia mafanikio ambayo kituo kimeyapata tangu kilipoanza. Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na ;-
- Kuweza kufanya marekebisho ya jengo la taasisi ya udhibiti wa viumbe hai waharibifu
- Kuweza kujenga jengo kubwa moja lenye ofisi, Maabara, kumbi za mikutano pamoja na darasa la kujifunzia wanafunzi wa elimu ya juu.
- Kuweza kujenga jengo dogo la kutunzia Wanyama (Animal House)
- Kuweza kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa shahada ya umahili na uzamivu kutoka nchi tofauti Africa
- Kutumia panya kwenye teknolojia za unusaji mfano kuweza kubaini vimelea vya kifua kikuu na harufu za mabomu yaliyotegwa ardhini.
Alipokuwa akizungumza na Uongozi na Watafiti wa Chuo hicho mara baada ya kupokea mawasilisho ya utekelezaji wa fedha zilizotolewa na Benki hiyo katika utekeelezaji wa miradi kwenye kituo cha umahiri cha mashariki na kusini mwa Afrika cha kudhibiti panya na matumzi yake katika kunusa (ACE IRPM & BTD) na miradi mingine inayofadhiliwa na Benki ya dunia Bwana Belete amesema;-
“Kwa kutambua mchango wa elimu kama mtaji wa binadamu ndio maana Benki ya Dunia tumeweka swala la elimu kama kipaumbele kwenye utekelezaji wa miradi yetu hivyo nitumie nafasi hii kuahidi Wizara ya Elimu pamoja na SUA kuwa tutaendelea kutoa ushirikiano katika kuteleza miradi kama hii ambayo inaleta tija kubwa kwenye maendeleo ya wananchi na Taifa”
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Dkt Keneth Hosea akitoa salamu za Wizara ya Elimu ameiomba Benki ya Dunia kuona uwezekano wa kuongeza fedha kwenye miradi hiyo ili kazi nzuri iliyofanywa na miradi kwenye vituo hivyo vya umahiri iendelezwe zaidi.
Awali Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda amesema mchango wa miradi hiyo miwili ya SACIDS na (ACE IRPM & BTD iliyofadhiliwa na Benki ya Dunia ni mkubwa sio tuu kwa Tanzania bali kwa bara la Afrika kwani tafiti zake zinagusa Afrika.
Katika mkutano huo Chuo kilipata nafasi ya kutoa mawasilishao mbalimbali ikiwemo Historia, Kazi na mafanikio ya Chuo toka kuanzishwa kwake iliyowasilishwa na Naibu Mkamu Mkuu wa Chuo Taaluma Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala ambaye alieleza namna Chuo kinavyotekeza majukumu yake.
Aidha, Mawasilisho mengine ni Utekelezaji wa Taasisi ya afya moja inayoshughukikia magonjwa ambukizi kusini mwa jangwa la Sahara (SACIDS) lililowasilishwa na Prof. Gerald Misinzo, Wasilisho la Mradi wa HEET lililowasilishwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango Utawala na Fedha Prof. Amandus Mharwa na Mratibu wa Mradi huo Dkt. Winfred Mbungu .
Baada ya mawasilisho hayo Mkurugenzi huyo Mkazi wa Benki ya Dunia Nchini Tanzania Bw. Nathan Belete pamoja na wajumbe wake walipata nafasi ya kutembelea kuona vituo hivyo na kazi zinazofanyika na kuona namna fedha walizotoa zilivyosaidia kufanyika kwa tafiti zenye faida kubwa kwa taifa na Afrika.